Marekani imesema iko "tayari kujadiliana na Iran bila masharti" baada uhasama uliozuka baina ya nchi hizo kufuatia mauaji ya jenerali Qasim Soleimani.
Katika waraka wake kwa Umoja wa Mataifa, Marekani ilijitetea kuwa ilimuua jenerali wa jeshi la Iran Qasem Soleimani kama hatua ya kujilinda. Iran ilijibu hatua hiyo kwa kushambulia kwa makombora kambi ya majeshi ya Marekani nchini Iraq japo hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Jenerali Soleimani ilichukuliwa kuwa afisa wa pili wa ngazi ya juu nchini Iran.
- Iran yashambulia kwa makombora kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq
- Gharama za mafuta zapanda baada ya mashambulizi Iraq
Kama mkuu wa kikosi maalum cha Quds Force, katika jeshi la ulinzi la Revolutionary Guards' alilikuwa mtekelezaji wasera za Iran katika eneo la mashariki ya kati.
Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Khamenei amesema shambulio hilo lilikuwa "kofi la usoni" kwa Marekani na kutoa wito kwa nchi hiyo kuondoka mashariki ya kati.Shambulio dhidi ya Soleimani pia liliwaua wanachama wa kundi la waasi wanaounga mkono Iran ambao pia wamesema watalipiza kisasi.
Hata hivyo, makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ameimbia kituo cha habari cha CBS kwamba "ujasusi" unaashiria kuwa Iran imewaambia waasi hao ambao ni washirika wake wasishambulie ngome zozote za Marekani.
"Tunapokea taarifa za ujasusi za kutia moyo kwamba Iran inatuma ujumbe kwa baadhi ya waasi kutoshambulia ngome za Marekani ama raia, na tunatarajia wataendelea kutoa ujumbe huo," Bw Pence aliambia kituo hicho.
Bunge la wawakili baadae leo Alhamisi linajiandaa kudhibiti uwezo wa rais Donald Trump kuanzisha vita dhidi ya Iran bila idhini maalum kutoka kwa Congress.
Maneno ya Rais Trump Jumatano ya Jana
Rais alitishia hatua ya kijeshi dhidi ya Iran ikiwashambulia maafisa wake au kambi yao, lakini hakutangaza hatua yoyote ya kijeshi, akisema kuwa shambulio la Iran halikusababisha majeruhi yoyote.
"Hakuna Mmarekani yeyote aliyejeruhiwa katika shambulio lililofanywa na utawala wa Iran, usiku wa kuamkia jana ," alisema.
"Iran inaonekana kurudi nyuma, hatua ambayo ni nzuri kwa pande zote husika," aliongeza.
Pia alisema kwamba "Marekani ina uwezo mkubwa kijeshi na kiuchumi, hali ambayo inaifanya kuheshimika". "Japo tuna zana za kijeshi za kisasa na zilizo na uwezo mkubwa wa kivita, haimaanishi lazima tuzitumie."
Barua kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Katika barua iliyotumwa kwa baraza la usalama la Umoja wa mataifa, balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Kelly Craft alisema Marekani iki tayari kufanya mazungumzo na Iran "kwa lengo la kuzuia hatari itakayoathili amani na usalama wa kimataifa".
Mauaji wa Soleimani yalistahili, barua hiyo ilisema, chini ya kifungu nambari 51 ya sheria ya umoja wa mataifa, inailazimu nchi "kuripoti mara moja" kwa baraza la usalama hatua yoyote ambayo imechukua katika haki ya kujilinda.
Awali Rais wa Marekani Donald Trump alisema Iran "inaonekana kurudi nyuma"baada ya kufyatua makombora dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Iraq.
Bw.Trump, alisema kuwa hakuna raia wa Iraq au Marekani aliyeuawa katika shambulio hilo japo kambi hizo ziliharibiwa kidogo.
Kambi za kijeshi za Irbil na Al Asad zilishambuliwa mapema Jumatano alfajiri.
Iran ilisema ilichukua hatua hiyo kulipiza kisasi mauaji ya wiki iliyopita ya jenerali wake wa ngazi ya juu Qasem Soleimani.
Ndege ya Marekani isiyokuwa na rubani ililenga msafara wake akiwa na maafisa wa wakuu wa kundi la waasi wanaoungwa mkono na Iran,mjini Baghdad katika hatua ambayo ilizorotesha uhusiano kati ya Iran na Marekani.
Comments