UN nayo haijanyamazia hatua hizi zinazoendelezwa na wababe wa dunia
Kutokana na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi kuhusu mvutano huo wa Syria, mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa utafanyika baadae leo. Mkutano huo utakuwa wa faragha.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hadi sasa Baraza la Usalama la umoja huo limeshindwa kufikia makubaliano ya kidiplomasia kuhusu Syria na amezitaka nchi wanachama wa kudumu wa baraza hilo kufikiria upya kwa kina na kuchukua hatua zitakazofaa ambazo hazitaongeza zaidi makali katika mzozo wa Syria.
Nchi hizo ni pamoja na Marekani, Urusi, China, Ufaransa na Uingereza. Urusi na Marekani hadi sasa zimepiga kura ya turufu kupinga azimio la kila mmoja la kutaka kuanzisha uchunguzi wa kimataifa kuhusu matumizi ya silaha za sumu.
Jana jioni Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, Mike Pompeo walikutana katika Ikulu ya Marekani kujadiliana kuhusu hali ya mambo inavyoendelea na kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua.
Donald Trump akiwa na Theresa May
Trump na viongozi wa mataifa ya Magharibi wameapa kuchukua hatua haraka kujibu shambulizi hilo la sumu lililofanyika kwenye mji wa Douma siku ya Jumamosi, ambapo wafanyakazi wa mashirika ya uokozi wamesema zaidi ya watu 40 waliuawa.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Thereza May, ameitisha leo kikao cha dharura cha baraza la mawaziri, kujadiliana iwapo ijiunge na Marekani na Ufaransa na kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria. May amesema Uingereza inataka kushiriki katika mashambulizi yoyote yatakayoongozwa na Marekani nchini Syria.
Amesema matumizi ya silaha za sumu ni jambo ambalo haliwezi kufumbiwa macho. ''Naam, mashambulizi ya silaha za sumu yaliyotokea Jumamosi huko Douma, Syria yalikuwa ya kutisha na ya kikatili. Imegharimu maisha ya watu wengi, wakiwemo watoto wadogo,'' alisema May.
Aidha, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron pia anatarajia kuamua kuhusu hatua za kuchukua katika siku zijazo, huku akisisitiza kwamba hataki mzozo wa Syria uongezeke na kwamba hatua yoyote ile itakuwa ni kujibu matumizi ya silaha za sumu na sio kuwalenga washirika wa serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu, OPCW, limesema hivi karibuni litapeleka timu yake ya wachunguzi kwenye mji wa Douma kwa ajili ya kufanya uchunguzi, lakini maafisa wa Marekani wamesema wanafanya kazi kwa kuzingatia taarifa zao wenyewe na hawatorudi nyuma.
Hayo yanajiri wakati ambapo Urusi imesema kuwa bendera ya Syria inapepea katika mji wa Douma, hali inayoashiria kuwa vikosi vya serikali vimechukua udhibiti kamili katika mji wa Ghouta Mashariki.
Nalo shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake London, Uingereza, limesema kuwa waasi waliokuwa wamebakia Ghouta Mashariki wamesalimisha silaha zao za kivita na kiongozi wao ameondoka katika ngome hiyo kuelekea eneo la kaskazini.
Katika hatua nyingine, shirika la ndege la Kuwait leo limesitisha safari zake za ndege kwenda Beirut kutokana na hofu ya usalama, baada ya shirika linalofuatilia usalama wa anga kuonya uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya anga nchini Syria katika siku zijazo.
Comments