Leo April 19, 2018 Meneja wa Fedha wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Prosper Kimaro amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kujilimbikizia mali zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.4 zisizolingana na kipato chake halali.
Kimaro anadaiwa kumiliki nyumba zenye thamani ya Bilioni 1,178,370,334, zilizopo maeneo ya Temeke DSM na magari 7 yenye thamani Shilingi Milioni 307,364,678.20.
Kimaro amesomewa mashtaka yake na wakili wa serikali, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja.
Wakili Vitalis amedai mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kujilimbikizia mali zisizolingana na kipato chake ambapo anadaiwa amelitenda kosa hilo kwa miaka tofauti kati ya 2012 na 2016.
Anadaiwa mali hizo amejilimbikizia maeneo ya Temeke DSM akiwa mtumishi wa umma wa TPA kama Meneja wa Fedha, amekutwa na mali zisizolingana na kipato chake halali cha zamani na cha sasa.
Mali hizo ni nyumba 2 zilizopo mtaa wa Uwazi Temeke (Mil 124.2), kiwanja kimoja kilichopo Yombo Vituka (Mil.12.9), nyumba 2 zilizopo Temeke (Mil 63.5).
Pia nyumba nyingine 3 zilizopo Temeke zenye thamani ya (Mil.159), nyumba nyingine 3 zilizopo maeneo hayo (Mil 170.1), nyumba nyingine moja (Mil 71.3).
Pia ana kiwanja Temeke (Mil 35), kiwanja kingine (Mil 25) na kujenga nyumba 3 (Mil 159), pia nyumba nyingine moja (Mil 106), pia nyumba nyingine 3 zilizopo Temeke zikiwa na thamani ya (Mil 214).
Pia ana nyumba 4 zilizopo Viziwa Ziwa Kibaha Mjini (Mil 199.7), nyumba nyingine Kilimahewa Tandika (Mil 70).
Pia anamiliki magari aina ya Toyota Land cruise (Mil 180.1), Mitsubishi (Mil 38.4), Massey Ferguson (Mil.24), Trailer (Mil 4.5), Toyota Harrier (Mil 35.8), Trailer (Mil 4.8), Massey Ferguson (Mil 19.1).
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana makosa yake ambapo Wakili Vitalis amedai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, pia hana pingamizi na dhamana.
Hakimu Simba ametoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini 2 watakaowasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh.Mil 200, pia mshtakiwa asitoke nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali pamoja na kuwasilisha hati zake za kisafiria.
Mshtakiwa huyo hajatimiza masharti ya dhamana, ambapo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi May 3,2018.
Comments