KESI YA WABUNGE 8 CUF BADO NI NGANGALI.
Waraka wa BASHIR YAKUB.
+255784482959
Ili wafanikiwe walitakiwa kutumia nafasi kuu tatu. Mosi kufungua kesi na kuzuia kikao cha nidhamu cha Cuf . Pili kufungua kesi kuizuia tume ya uchaguzi kuidhinisha kufutwa na uteuzi wabunge wapya. Tatu kufungua kesi kulizuia bunge kuwaapisha wabunge wapya wateule.
1.KUZUIA KIKAO CHA NIDHAM CHA CUF .
Kesi nzuri ilitakiwa kufunguliwa mara tu baada ya kupata wito wa kikao cha nidhamu. Hapa wangeweza kufungua kesi kwa hati ya dharula na kufanya maombi madogo ya zuio la muda(temporally injunction).
Wangezuia kikao cha nidhamu cha Cuf na katu kisingefanyika.
2. KUIZUIA TUME YA UCHAGUZI.
Lakini kama wangeshindwa kuzuia kikao cha Cuf pengine kwa kuchelewa ama vinginevyo bado walikuwa na nafasi ya kufungua kesi na kuomba zuio dhidi ya Tume ya uchaguzi kuidhinisha kufutwa kwao kwa mujibu wa Ibara 78(4) ya katiba inayosomwa na kifungu cha 86(8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Wangeomba zuio la kuzuia kuidhinisha kufutwa kwao na kuzuia uteuzi wa wabunge wapya.
3. NAFASI WALIYOBAKI NAYO.
Wabunge hawa 8 wamebaki na nafasi moja. Ni kulizuia bunge kuwaapisha wabunge wapya katika bunge lijalo September, 5 , 2017.
Hata hivyo hatua hii ni ngumu na pengine itakayoshindwa. Mnakumbuka November , 27, 2014 wakati Jaji Razia Sheikh, Richard Mziray na Lugando Mwandambo walipotoa zuio kulizuia bunge kujadili ripoti ya Escrow.
Bunge lilikataa kwa kutumia ibara ya 100 ya Katiba inayotoa mamlaka kwa shughuli za bunge kutoingiliwa na chombo kingine chochote. Zuio hilo halikusaidia kwani ripoti hiyo iliwasilishwa kama ilivyokuwa imepangwa.
Hii si Tanzania tu, bali hata juzi mtakuwa mlimsikia Spika Rebecca Kadaaga wa Uganda akiikataa amri ya mahakama iliyolizuia bunge kuwahoji maafisa 42 kwenye kashfa ya bilioni 6 wanazodaiwa kupewa zawadi na Museveni.
Kwahiyo hatua hii ni ngumu na pengine isiyowezekana. Nafasi mbili walizopoteza kwa kushindwa kuzuia vikao vya Cuf na tume hakika zitakuwa zimewagharimu.
4. NINI KITAFUATA.
Hatua zote za kufutwa na kuteua zimeshapitiwa isipokuwa imebaki moja tu. Imebaki wabunge wapya kuapishwa hapo September 5 bunge litakapofunguliwa.
Kuna kesi Kisutu lakini tumeona ugumu wa kuzuia hatua hii ya kuapishwa. Kwahiyo kwa haraka tunaweza kusema kuwa wataapishwa na watakuwa wabunge.
5. JE KESI WALIYOFUNGUA ITAKUFA.
Hapana itaendelea. Wanachoomba pamoja na mambo mengine ni mahakama kubatilisha mchakato wa kufutwa kwao na uteuzi wa wabunge wapya.
Wanaweza kufanikiwa au wasifanikiwe. Changamoto kubwa wanayokabiliana nayo hapa ni mda. Kesi yao inafunguliwa Kisutu na hapo itakaa muda.
Kwa vyovyote itavyokuwa yeyote atakayeshindwa hakuna shaka atakata rufaa mahakama kuu. Na hapo itakaa muda.
Kwa vyovyote itakavyokuwa yeyote atakayeshindwa hakuna Shaka atakata rufaa kwenda mahakama ya rufaa. Na hapo itakaa muda.
Kwa hesabu ya haraka hapo hatuongelei chini ya miaka miwili ama mitatu kukamilisha mchakato huo wote. Na bado hakuna guarantee kwamba lazima washinde wao. Yeyote anaweza kushinda.Wakati huohuo 2020 imebakiza takribani miaka miwiii na nusu hivi ili bunge livunjwe.
Unaweza kuona ni kwa kiasi gani wamepoteza.
6. KWANINI WAMEPOTEZA.
Tatizo ni kumdharau LIPUMBA. Kwa mtu makini huwezi hata kidogo kumdharau mtu (1) aliyerudia uenyekiti wake baada ya kujiuzulu na akafanikiwa (2) akaichukua ofisi kuu buguruni na kufanikiwa(3) akalifuta baraza la wadhamini na kusajili lake na akafanikiwa (4)na sasa amefuta wabunge.
Mtatiro anasema LIPUMBA ni wa kupuuza. Kweli mtu wa aina hii ni wa kupuuza ??!. Kama utampuuza mtu wa aina hii basi wewe utashughulika na mtu wa aina gani.
Mtatiro na wenzake wanasema LIPUMBA amechangayikiwa . Kweli kwa kipimo cha akili haya matukio ya LIPUMBA ni ya uchizi!!!. Kama mtu anaweza kuchanganyikiwa hivi basi ipo haja ya kusali na kuomba uchizi wa aina hii.
Maneno ya kumpuuza waliyohubiriwa na Mtatiro yaliwafanya wabunge hawa wampuuze kweli . Na sasa mnakimbizana na vikao vya dharula huko Zanzibar kwa mtu mliyekubaliana kumpuuza , extremely and hopelessly too late.
Nadhani badala kuwahubiria kumpuuza LIPUMBA ilitakiwa kuwaambia wafuasi wenu kuwa, "Kuweni makini na LIPUMBA , na kila hatua anayoichukua imebebeni kwa uzito na haraka ijibuni kwa hatua nyingine ya kisheria" . Pengine yasingewakuta hawa wabunge.
Yote kwa yote Poleni.
Comments