Miujiza ya mbegu za pera kwa kinamama
WAWEZA kuita ni miujiza. Wakati walaji wengi wa mapera wakiwa na kawaida ya kuondoa mbegu, imefahamika kuwa kufanya hivyo ni kosa kubwa kiafya kwa sababu wahusika hujikosesha faida nyingi kiafya.
Uchunguzi unaohusisha mahojiano na madaktari pamoja na maandiko mbalimbali ya utafiti wa lishe, umebaini kuwa ulaji wa mbegu za mapera, iwe kwa kuzisaga na kunywa kupitia juisi au hata kuzimeza bila kuziponda zina manufaa na zina miujiza mingi katika kuukinga mwili dhidi ya magonjwa.
Baadhi ya virutubisho vilivyomo kwenye pera na pia mbegu za tunda hilo ni pamoja na kiwango cha juu cha vitamin A, vitamin C, vitamin E na madini yakiwamo ya niacin, thiamine, chuma, calcium, potassium, phosphorus na manganese. Pia kuna kiasi kikubwa cha kinga dhidi ya vijisumu.
Faida zake mwilini ni pamoja na kupunguza uwezekano kwa mlaji kupata saratani ya tezi dume; kisukari; saratani ya matiti; maradhi ya shinikizo la damu; tumbo kuvimba kwa sababu ya chakula kutosagika vizuri; kusaidia ngozi kuwa nyororo; kuzuia nywele kupukutika hivyo na pia kuzifanya ziwe laini.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Nipashe imebaini kuwa mbegu za pera pia husaidia kuimarisha afya ya uzazi kwa walaji wake.
Mbegu za pera huwasaidia walaji kuwa na uwezekano mdogo wa kupata tezi dume, hiyo ikitokana na uwezo wake wa kuzuia ukuaji wa seli za saratani kwa kuwa na kinga iitwayo ‘lycopene’. Inaelezwa vilevile kuwa mbegu za tunda hilo husaidia kuzuia kansa ya matiti.
Miujiza mingine ya mbegu za pera ni kusaidia udhibiti wa lehemu katika mwili wa mlaji, kuzuia nywele kupukutika kwa kuzifanya ziwe laini na imara.
Akizungumza na Nipashe, mtaalamu wa lishe, Dk. Amani Assey, alisema mbegu za pera zina faida nyingi ikiwamo ya kuwasaidia kina mama wenye matatizo ya kutoona siku zao za mwezi.
“Ikiwa mwanamke hajapata siku zake kwa muda mrefu au zinajirudia kwa mwezi, mbegu za mapera ni dawa nzuri kwake,” alisema Dk. Assey.
Akifafanua, Dk. Assey alisema kinamama wenye matatizo kuhusiana na siku zao wanashauriwa kunywa juisi ya mapera kwa miezi mitatu mfululizo ili madini yaliyomo kwenye pera yaende kushtua homoni za mwili. Pia alizungumzia namna mbegu za pera zinavyosaidia kudhibiti kisukari.
“Ngozi iliyopo kwenye mbegu ina uteute ambao ukiingia tumboni unabaki na humsaidia kumkinga na ugonjwa huo (kisukari). Ulaji (usiozingatia taratibu) huwaweka baadhi ya watu katika hatari ya kupata kisukari. Ila kutumia mapera mara kwa mara kutamwepusha (mtu) kupata kisukari, “ alisema Dk. Assey.
Kadhalika, alisema ulaji wa pera humwezesha mtu kupata madini ya shaba ambayo huenda kuimarisha ufanyaji kazi tezi ziitwazo thyroid.
Alisema ndani yake kuna vitamini B3, vitamini B6 ambazo husaidia kuimarisha afya ya akili.
“Unywaji wa juisi ya pera kwa wale wanaosumbuliwa na maumivu ya tumbo au kukaa muda mrefu bila kupata choo ni muhimu kwa sababu kutamsaidia (mhusika) kuondoa uchafu uliopo,” alisema Dk. Assey.
Aidha, mbegu za mapera huwasaidia zaidi pia kinamama pindi wanapokabiliwa na tatizo la kutoona siku zao (hedhi) kwa usahihi.
Daktari Seleman Hassan wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, aliiambia Nipashe kuwa mbegu za pera husaidia ufanisi wa mifumo mingi mwilini na ndiyo maana wanawake wenye matatizo ya hedhi hupata nafuu kwa kula mbegu za matunda hayo.
Pia alisema mbegu hizo zimejaaliwa kuwa na viondoa sumu mwilini na kumkinga mtu na maradhi ya saratani ya tezi dume, saratani ya matiti na saratani ya midomo.
Kadhalika, alisema watumiaji wa mbegu hizo hunufaika kwa kudhibiti uzito wa miili yao kwa wale wenye uzito mkubwa na pia kuwa na kumbukumbu nzuri.
“Zina vitamin A kwa wingi ambayo inasaidia macho kuona vizuri. Pia walaji wa mbegu za mapera hupata kinga dhidi ya mafua, kikohozi, na kuharisha,” alisema Dk. Hassan.
MAAJABU ZAIDI
Pera pia lina maji na kambakamba ambazo ni muhimu pia kwa afya. Pia husaidia mmeng’enyo wa chakula na kuwa na viinilishe vyenye kuukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali yakiwamo ya saratani, kupunguza uwezekano wa mlaji kupata maradhi ya kisukari, kuimarisha afya ya uzazi kwa kusaidia urutubishaji wa mbegu miongoni mwa wapendanao na pia kutibu maumivu ya tumbo, tumbo kuvimba kutokana na chakula kutosagika vizuri, kuendesha na pia kiungulia. Kadhalika, matumizi ya mara kwa mara ya juisi ya pera pamoja na mbegu za tunda hilo huwasaidia walaji kuwa na ngozi nyororo.
Comments